Barua ya Zitto kuhusu Lwakatare:
Nimetafutwa na uongozi wa JamiiForums ili kutoa maelezo kuhusu
barua iliyowekwa jukwaani inayoonyesha kuwa ndani ya chama kuna
kutoelewana kuhusiana na msimamo juu ya kesi inayomkabili mmoja wa
viongozi waandamizi wa chama Ndg. Wilfred Lwakatare, Mkurugenzi wa
Ulinzi na Usalama wa chama.
Maelezo yangu ni kama ifuatavyo:
1. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa chama mnamo tarehe 15 Machi
2013 kutaka chama kifanye uchunguzi wake wa ndani kuhusiana na ukweli wa
video iliyowekwa kwenye mitandao inayoonyesha kuwa Kiongozi wetu
mwandamizi anapanga mipango ya kumdhuru Mhariri wa moja ya magazeti hapa
nchini. Sikuamini kabisa mambo yale na hivyo kutoa ushauri kwa chama
kwamba tufanye uchunguzi wetu wa ndani ili kujiridhisha. Uchunguzi wa
ndani ungetufanya kuweka mikakati wa namna bora zaidi ya kulinda chama
dhidi ya njama zozote, za ndani au za nje ya chama.
2.
Mapendekezo yangu ndani ya chama kamwe hayakulenga kumtosa ndugu
Lwakatare wakati huu anakabiliwa na changamoto hii bali yalilenga
kuhakikisha kuwa wakati tunamlinda na kumtetea ili haki itendeke, lazima
tuhakikishe kuwa chama hakitaathirika na sakata hili kwa namna yeyote
ile. Ni jukumu letu kuhakikisha sura (image) ya chama inabakia salama
maana hatujui mikakati (game plan) ya maadui zetu kisiasa hasa baada ya
kauli zao kwamba chama kitakufa kabla ya 2015 ambayo imerudiwa rudiwa
sana. Ni lazima kutilia shaka (doubt) kila linalotokea sasa kwa kulipima
kwa jicho la mbele zaidi. Ikumbukwe maneno ya Mwenyekiti wetu
“Mwenyekiti Freeman Mbowe anataka ikithibitika kuwa Lwakatare alishiriki
kurekodi mkanda huo iwe kwa kurubuniwa, ‘kushikishwa’ au kuingizwa
mkenge, itamlazimu kuwajibika kwa kosa la kukosa umakini” (Gazeti la
Jamhuri).
3. Barua ile ya tarehe 15 Machi 2013 ilikuwa ni
ya ndani ya chama, haikuwa ya kiofisi bali ya Zitto Kabwe kwa chama,
ilisainiwa na haikukusudiwa kuwa ‘public’. Nimeshangazwa sana kusikia na
baadaye kuona barua yenye maudhui kama yale yale ya barua yangu kwa
Katibu Mkuu imewekwa mtandaoni. Barua imewekwa masaa machache baada ya
kikao cha Kamati Kuu kwisha ambapo tuliweka msimamo wa pamoja wa chama
juu ya namna bora ya kushughulikia suala la Lwakatare kama chama. Wakati
mweka barua anadai kuwa kulikuwa na mgawanyiko katika kikao, ukweli ni
kwamba ajenda hiyo haikuwa na mjadala wenye mgawanyiko kabisa na msimamo
wa chama ulipatikana kwa mwafaka bila mgawanyiko. Ni dhahiri kuwa
maadui zetu walitaraji mgawanyiko na baada ya kushindwa sasa
wanatengeneza mgawanyiko huo kwa kusambaza uwongo wenye uzandiki.
4. Baada ya kufanya uchunguzi mdogo nimegundua kuwa ID iliyoweka
video ya Lwakatare mtandaoni na ID iliyoweka barua hii mtandaoni ni IDs
za mtu mmoja. ‘Coincidence’ ya namna hii inashangaza na kushtusha,
lakini inatuambia jambo moja kubwa ‘kwamba kuna kirusi ndani ya chama
kilicho karibu sana na viongozi wa chama chenye kazi moja tu, yani
kuonyesha kuwa CHADEMA hapako shwari, kuna migogoro na hatimaye
kusambaratisha chama’. Kirusi hiki lazima kina nafasi andamizi au kipo
karibu sana na viongozi waandamizi. Inawezekana kabisa kirusi hiki
kinahusika na suala zima la Lwakatare katika kupanga, kuendesha na
kutekeleza mpango mzima. Maswali kama ‘kwanini Dennis Msacky na Zitto
ndani ya Video ya ‘Lwakatare’ lazima sasa yaanze kutafutiwa majawabu.
5. Natoa wito tena kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kwamba, huu
ni wakati wa kuwa na umoja na mshikamano kuliko wakati wowote ule
katika uhai wa chama chetu. Chama cha Mapinduzi kitatumia njia zote
kutugawa, kutugombanisha na kupenyeza chuki miongoni mwetu katika juhudi
za wao kubakia madarakani. Umakini wa Kiongozi huonekana wakati wa
changamoto kama hizi!
6. Msimamo wa chama umetolewa na
Kamati Kuu iliyomaliza vikao vyake jana siku ya ijumaa tarehe 5 Aprili
2013. Huo ndio msimamo wangu pia! Kesi ya Lwakatare ipo mahakamani,
chama kimeonyesha dhahiri kumwamini Jaji aliyekabidhiwa kesi hii, sasa
tuache mahakama ifanye kazi yake na tusubiri hukumu. Msemaji wa chama
kuhusu suala hili ni ndugu Tundu Lissu na amekuwa akitoa ufafanuzi kila
inapohitajika.
Asanteni
credit:Habari Mpasuko
Saturday, April 6, 2013
Post a Comment