Loading...

Tuhuma za kuua zazidi kuwaandama Polisi

Na mbeyayetu.blogspot.com


Jeshi la polisi mkoani Mbeya limeendelea kujisiriba matope kwa kuendesha mauaji ya kiholela kwa raia ambapo jana askari wa jeshi hilo wamemuua mwanafunzi Said Msabaha wa shule ya Sekondari Lupa iliyopo wilayani Chunya mkoani hapa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupa wilayani humo William Patrick Mbawala, ameuambia mtandao huu kuwa mwanafunzi huyo kabla ya kifo chake alikamatwa na askari hao akiwa na wenzake watatu kwa tuhuma za wizi wa simu Februari 29, mwaka huu na baadaye waliachiwa kwa dhamana.

Amesema baada ya kutolewa katika kituo kidogo cha Lupa, Marehemu alionekana kuwa hali yake imedhoofika na alipoulizwa alieleza kuwa alipokuwa kituoni hapo alipigwa na askari polisi jambo ambalo liliwalazimu kumpeleka katika zahanati ya kijiji hicho chini ya Mganga aliyemtaja kwa jina la Dr. Solomon.

Amesema Baada ya kuona hali yake inaendelea kuwa mbaya ndipo lilipochukuliwa jukumu la kumpeleka Hospitali ya wilaya na bahati mbaya akafia njiani hata kabla ya kumfikisha katika Hospitali hiyo.

Naye Baba mzazi wa marehemu, Msabaha Hussein, amesema kuwa baada ya kufariki mtoto wake akachukua jukumu la kupeleka maiti kituo cha polisi ili wahusike katika kuuzika mwili wa marehemu kwa kile aichodai kuwa kifo cha mwanae ni matokeo ya kipigo walichokitoa alipokuwa mikononi mwao.

Nao baadhi ya wananchi waliohojiwa kwa masharti ya kuhifadhi majina yao wamesema kuwa baada ya kuona hali hiyo na kwasababu askari wanaodaiwa kuhusika wanawafahamu ndipo walipochukua jukumu la kuwatafuta askari hao ambao tayari walikuwa wametokomea kusikojulikana.

Wamesema kuwa baada ya kuwakosa katika makazi yao, waliamua kuzichoma moto nyumba za askari hao ambao ni Copl. Maxmillian, PC Mjuni na PC Hery ambapo hawakuishia hapo walimtafuta PC Fadhil bila mafanikio na kuharibu samani zake za ndani huku wakishinikiza Jeshi la polisi kuuzika mwili wa marehemu huyo.

Afisa upepelezi wa Jeshi hilo mkoani Mbeya (RCO) Elias Mwita alipotakiwa kuzungumzia sakata hilo alisema kuwa ni mapema mno.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Chunya Deodatus Kinawiro ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo alipotafutwa ili aweze kuzungumzia tukio hilo hajaweza kupatikana kupitia simu yake ya kiganjani.

Awali askari hao walidaiwa kutorokea Jijini Mbeya lakini taarifa kutoka ndani ya vyanzo vya kikosi kazi cha mtandao huu jeshi la Polisi mkoani Mbeya vimesema kuwa askari hao walikuwa bado hawajakamatwa wala kuonekana katika viunga vya Jiji la Mbeya.

Tukio hilo la kinyama limetokea siku chache baada ya askari wa jeshi hilo PC Maduhu kuhusika kumuua aliyekuwa Mwanafunzi wa chuo kikuu cha TEKU kilichopo jijini mbeya Daniel Godluck Mwakyusa (31) February 14, mwaka huu.

Habari na Ezekiel Kamanga, Chunya.



Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top