Mohamed Mandindo (36) mkazi wa kijiji cha Chingurunguru kilichopo katika wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma amekufa papo hapo na mwingine amejeruhiwa vibaya baada ya pikipiki zao waliokuwa wakiziendesha kugongana uso kwa uso.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimeki amemtaja aliyejeruhiwa vibaya kuwa ni Alex Kiwanga (26) mkazi wa kijiji hicho ambaye kwa sasa amelezwa katika hospitali ya serikali ya wilaya ya Tunduru ambako anaendelea kupata matibabu.
Kamanda Msimeki alifafanua zaidi kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 6:00 mchana huko katika kijijicha Chingurunguru kwenye barabara itokayo Tunduru kuelekea wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.
Alisema kuwa inadaiwa siku ya tukio pikipiki yenye namba za usajili T748 AAE aina ya honda ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Kiwanga iligongana uso kwa uso na pikipiki yenye namba za usajili T251 BHL aina ya SanLg iliyokuwa ikiendeshwa na Mandindo aliyekuwa akitoka kwenye kijiji cha Chingurunguru kuelekea Tunduru mjini.
Alibainisha zaidi kuwa Kiwanga alikuwa akitokea Tunduru mjini kuelekea Chingurunguru akiwa kwenye mwendo mkali ghafla aliiona pikipiki nyingine mbele yake ambayo nayo ilikuwa kwenye mwendo mkali na kusababisha kugongana ambapo Mandindo alikufa papo hapo na Kiwanga alijeruhiwa vibaya na alikimbizwa kwenye hospitali ya serikali ya wilaya ya Tunduru ambako amelazwa huku akiwa anaendelea kupatiwa matibabu zaidi.
Hata hivyo kamanda Msimeki alisema chanzo cha ajali hiyo kimesababishwa na mwendo mkali wa pikipiki ambazo madereva walishindwa kumudu usukani wa pikipiki zao.
Post a Comment