MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Chande Nalicho ameliagiza Jeshi la polisi kumsaka na kumkamata Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkowela Mohamed Mkopi ili kujibu tuhuma za kuingiza Ng’ombe bila ridhaa ya wananchi wa kijiji hicho.
Agizo hilo alilitoa jana wakati akiongea na Wananchi katika maadhimisho ya Sikukuu ya wakulima Nanenane yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Nakapanya Wilayani humo.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho alisema kuwa maagizo hayo ameyatoa kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa afisa huyo aliandika kibali cha kuwaruhusu wafugaji wa kabila la Kisukuma kuingiza kundi la ng,ombe 270 mwanzoni mwa mwezi huu.
Sambamba na maagizo hayo Nalicho pia akatumia nafasi hiyo kuiagiza idara ya Mifugo Wilayani humo kufuatilia na kumpelekea takwimu za idadi ya makundi ya ng’ombe waliosambaa katika vijiji vya wilaya hiyo.
Aidha katika maagizo hayo Nalicho aliwaahidi wananchi hao kuwa baada ya kupokea takwimu hizo atafanya kikao na wataalamu kupitia miongozo na taratibu zilizo waruhusu wafugaji hao kuingia ovyo katika maeneo ya vijiji hivyo na kwamba wafugaji watakaobainika kuvamia
maeneo hayo bila idhini ya wananchi wataondolewa.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho alisema kuwa maelekezo hayo ameyatoa baada ya kubaini kuwa Wilaya yake hivi sasa inakabiliwa na migogoro na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima na Wafugaji huku kila upande ukidai kuwa na haki ya kufanya shughuli zake katika maeneo husika hali inayotishia kuzuka kwa mapigano kwa makundi hayo.
Aidha Nalicho pia akatumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kukopa matrekta ili yawasaidie kuondokana na kutegemea jembe la mkono na kuboresha kilimo chao pamoja na kuwataka wananchi kujitokeza bila uoga na kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya watu na makazi na kutoa maoni yao katika zoezi la utoaji wa maoni wakati wa kuandika Katiba mpya.
Awali akisoma Risala ya maadhimisho hayo Kaimu afisa Kilimo na Mifugo Wilayani humo Hasan Simba mbali na kukiri kuwepo kwa kero hiyo aliahidi kukusanya kwa haraka takwimu hizo ili kuisaidia Wilaya kuondokana na migogoro hiyo pamoja na kuwahamisha wafugaji hao katika maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za taifa wanakoripotiwa kuvamia.
Simba aliendelea kufafanua kuwa hadi sasa jumla ya wananchi 41 wa Wilaya hiyo wamejitokeza kuomba kukopa matrekta hayo ambapo kati yao 24 tayari wamekwisha katimiza taratibu zote na kulipia matrekita hayo kati ya matrekta 100 yaliyopelekwa na serikali Mkoani Ruvuma.
Nje ya viwanja vya mikutano hiyo wakulima Juma Mtukula, Joyce Mpugale na Mohamedo Swalehe wakapaza sauti zao kwa kuiomba Serikali kuandaa utaratibu madhubuti wa kuwatafutia wakulima masoko ya uhakika ya mazao yao pamoja na kupeleka pembejeo kwa wakati ili waweze kuendana na kauli mbiu ya kilimo kwanza.
Post a Comment