Na Stephano Mango, Songea
WAZEE nchini wameitaka Serikali kutumia busara na hekima katika kutatua mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa ulioibuliwa kwa mara nyingine tena na viongozi wa nchi ya Malawi hivi karibuni na kusababisha hofu miongoni mwa jamii ya watanzania
Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu wa mtandao wa Kinga Jamii Tanzania Iskaka Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa
Msigwa alisema kuwa mgogoro huo toka umeibuliwa na nchi ya Malawi na viongozi wetu kuendelea kutoa matamko makali kuhusu jambo hilo kumeendelea kuzua hofu miongoni mwa jamii ya wazee, wanawake na watoto
“ Penye hofu na wasiwasi, hapana amani wala usalama miongoni mwa jamii kutakapopelekea ukosefu wa maendeleo hivyo ni lazima serikali ikawa makini kwa kujiimarisha kijeshi mipakani licha ya kuitaka jambo hili kumalizwa kwa busara kwani adui anayetuchokoza ana malengo na ajenda zaidi ya Ziwa Nyasa kama tunavyodhani"alisema Msigwa
Alisema kuwa Serikali inawajibika kumaliza mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo ili nchi hizo ziendelee na mahusiano yaliyokuwepo toka awali badala ya kufikiria vita ambavyo vitaleta maafa makubwa kwa wazee, wanawake na watoto kwani jambo hilo halihitaji kupimana ubavu
Alieleza kuwa inawezekana kabisa mgogoro huo ukamalizika pasipo umwagaji wa damu au upotezaji wa maisha ya watu kwa vita badala yake watumie busara kwa kuangalia ramani zilizopo kwenye taarifa mbali mbali za miaka ya enzi za ukoloni hasa zilizoko kwenye maktaba wakati Tanzania inaitwa Tanganyika; na Malawi inaitwa Nyasaland ukweli kuhusu mipaka yetu utapatikana.
Post a Comment