Loading...

WAISLAM WATAKIWA KUSHIKA MAFUNDISHO YA DINI


Na Stephano Mango, Songea

WAISLAM nchini wametakiwa kuhakikisha kuwa wanauendeleza uadilifu na mafundisho ya dini hiyo ili kudumisha amani na usalama wa watanzania na majirani zao hapa duniani ili kuweza kujenga jamii iliyo bora kiroho na kimwili.

Maombi hayo yalikuwa ni sehemu ya Ibada ya swala ya Idd el fitr iliyofanyika katika Msikiti wa mkoa wa Ruvuma uliopo mjini Songea iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini wa Dini hiyo wakiongozwa na mufti wa Tanzania Sheikh Issa Shaaban bin Simba na Mgeni Rasmi kitaifa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu.

Immam wa Msikiti huo, Sheikh Shaaban Mbaya katika maombi maalum ya kuliombea taifa na viongozi wake wapate afya njema na uwezo wa kuwatumikia watanzania ili wawe na amani, alisema kuwa waumini wa kiislamu hawatakiwi hata kidogo kumbagua muislam au asiye kuwa muislam katika maisha yao ya kila siku.

Alisema, mafundisho ya dini hiyo yana sisitiza upendo na amani ili kuenzi uumbaji wa mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa rehema na kwamba viumbe vyote vya ardhi, majini na hewani ameviumba yeye mwenyewe bila ubaguzi kwa manufaa ya viumbe kwakuwa vinategemeana.

Alieleza zaidi kuwa waumini hao wafuate mafunzo toka kiongozi wao, Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliweza kuwatunza mayatima na watu wasiokuwa na uwezo kiuchumi ambao wasiowaislamu na waislamu ili wapate furaha ya maisha yao ya kila siku licha ya shida na upweke waliokuwa nao.

"Ndugu waumini haina maana wakati huu wa sikukuu mkajipamba kwa nguo safi na mkala vyakula vizuri wakati mioyo yenu na matendo yenu hayampendezi mwenyezi mungu," alisema Immam Sheikh Shaaban Mbaya na kusisitiza kuwa ni vyema wakaona umuhimu wa kuendeleza mafundisho waliyoyapata mwezi Mtukufu wa ramadhani kwa manufaa ya watu wote.

Aidha, Sheikh Mbaya alisema, Uchoyo na tamaa za mali, matendo mabaya na uroho wa madaraka na kudhalilisha wengine ndiyo chanzo cha kuvuruga amani iliyopo kuanzia ngazi ya familia, kijiji wilaya taifa na kimataifa.


Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top