Loading...

TUME YA KATIBA YATOA WITO KWA WANAWAKE MKOANI RUVUMA

Na Stephano Mango, Songea

WANAWAKE mkoani Ruvuma wametakiwa kuhamasishana kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba ili waweze kutoa maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii zao

Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa kundi la tano la Tume ya mabadiliko ya katiba Profesa Mwesiga Baregu kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Seedfarm Villa mjini Songea

Profesa Baregu alisema kuwa kumekuwepo na idadi isiyoridhisha ya wanawake wanaohudhuria katika mikutano ya Tume kulinganisha na idadi ya wanawake waliopo kwenye kata hizo kwani takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu 8,915 waliojitokeza kuhudhuria mikutano ya Tume katika wilaya ya Namtumbo na Tunduru wanawake ni 1,949 tu ambao ni sawa na asilimia 21.9 ya mahudhuria

“ Hii ni idadi ndogo sana kwa akina mama kujitokeza kwenye mikutano hiyo muhimu kwa mustakabari wa wananchi na nchi kiujumla, hivyo Tume inawajibika kutoa wito ili waweze kujitokeza kwa wingi na kuchangia kutoa maoni yao kwa uwazi”alisema Profesa Baregu

Alifafanua kuwa pia kumekuwepo na idadi ndogo sana ya wanawake wanaojitokeza kutoa maoni katika mikutano ya Tume ukilinganisha na uwingi wao kwenye kata mbalimbali kwani takwimu tulizonazo katika Wilaya ya Tunduru na Namtumbo wananchi waliotoa maoni kwa njia mbalimbali ni 2,074 ambapo wanawake ni 198 tu idadi hiyo ni ndogo kulinanisha na wanawake 1,949 ambao wamehudhuria mikutano hiyo

Alieleza changamoto nyingine waliyokutana nayo ni idadi ndogo ya wananchi wanaochangia maoni ya mabadiliko ya katiba kwa njia ya kuongea au kwa kuandika kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika wananchi 8,915 waliohudhuria mikutano mbalimbali waliochangia ni 2,074 sawa na asilimia 23.3 ya waliohudhuria

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba Jaji Joseph Walioba alisema kuwa wananchi wengi wanaojitokeza kwenye mikutano ya Tume wamekuwa wakilalamika kwamba hawaielewi katiba iliyopo hivyo itakuwa vigumu wao kuchangia na kutoa maoni yao lakini mwananchi huyo anapoanza kutoa maoni yake anaeleza mambo ya msingi yanayohusiana na katiba
Jaji Walioba alieleza kuwa katika mkoa wa Ruvuma Tume inatarajia kufanya mikutano 72 katika jumla ya kata 72 zilizopo kwenye wilaya tano za mkoa wa Ruvuma ikiwemo wilaya ya Nyasa, Namtumbo, Mbinga, Tunduru na Songea


Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top