Loading...

Vioja kesi ya Lwakatare *Aachiwa, akamatwa tena papo hapo

Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam, ilimwachia huru Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph, kisha kuwakamata tena.

Baada ya Lwakatare na mwenzake kukamatwa tena, waliingizwa mahakamani kisha kusomewa upya mashtaka ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.

Washtakiwa hao waliachiwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Emilius Mchauro, baada ya kukubaliana na maombi yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri.

Washtakiwa waliingizwa katika chumba kidogo cha mahakama, huku wafuasi wa CHADEMA na wengine waliofika kusikiliza kesi hiyo wakisubiri kesi iingie katika mahakama ya wazi.
Lakini hadi wanatoka mahakamani, hakuna aliyekuwa akijua kama tayari watuhumiwa wamepandishwa kizimbani, wakiwemo mawakili wanaowatetea.

Mchauro, alitakiwa kutoa uamuzi wa kuwapa dhamana au la washtakiwa, lakini badala yake Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza amewasilisha hati (Nole) kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) ya kuonyesha kwamba hana haja ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

“Mheshimiwa, DPP amewasilisha nole chini ya kifungu cha sheria namba 98(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, akionyesha Jamhuri haina haja ya kuendelea na mashtaka hayo tunaomba yafutwe,” alidai Rweyongeza.

Hakimu Mchauro, aliyakubali maombi ya DPP na kuwaachia huru washitakiwa kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili.

Baada ya kauli hiyo, washtakiwa walitoka nje ya chumba kidogo cha mahakama na ghafla walikutana na polisi ambao waliwaamuru wawafuate.

“Nini, mnanikamata kwenda wapi, siendi kokote, mnakiherehere sana hadi mawakili wangu waje,” alidai Lwakatare huku akigoma kuondoka alipokuwa amesimama.

Lwakatare alishauriwa na watu waliozunguka katika eneo hilo, hadi alikubali kuwafuata askari ambao walimpeleka mahabusu ambako alikaa kwa saa moja, kisha kupandishwa tena kizimbani.

Lwakatare alisindikizwa na magari ya Polisi zaidi ya sita, gari moja kubwa lenye maji ya kuwasha na mbwa nane ambao miongoni mwao wametolewa nchini Lebanoni, walipokuwa wakifanya kazi za ulinzi.

Mbwa hao, majina yao ni PD Kambi, Giro, Simba, Kino, PD Roger. PD Ivo, PD Hudra na PD Boby, wote walikuwa wakitembezwa tembezwa nje ya jengo la mahakama kwa nia ya kuimarisha ulinzi.

Mbwa hao, walikuwa wakisogea katika kila kundi linalokusanyika na kulizingira huku wakibweka.

Washitakiwa walisomewa mashtaka upya na Wakili Rweyongeza mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana.

Akiwasomea mashitaka, Rweyongeza alidai washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne yakiwemo ya kula njama ya kumdhuru kwa sumu na kumteka Denis Msaki, Desemba 28 mwaka jana maeneo ya Stop Over Kimara.

“Shtaka la kwanza kwa ajili ya washitakiwa wote wawili, wanadaiwa Desemba 28, 2012, maeneo ya King’ong’o Kimara Stop Over walikula njama ya kutenda kosa la kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Denis Msaki.

“Shtaka la pili kwa washitakiwa wote, limefunguliwa chini ya kifungu cha sheria namba 24 (2) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, wanadaiwa walikula njama ya kumteka Denis Msaki kinyume cha sheria namba 4(2) aya (C) (iii) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.

“Mheshimiwa shtaka la tatu, linawakabili washitakiwa wote pia, wanadaiwa kinyume cha kifungu namba 5(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, kwa pamoja walifanya mkutano wa kufanya vitendo vya kigaidi, walipanga, walishiriki mkutano huo wenye lengo la kupanga kitendo cha ugaidi kwa kumteka nyara Denis Msaki.

“Shtaka la nne la kuhamasisha vitendo vya ugaidi, linamkabili mshitakiwa wa kwanza, Lwakatare, kwamba Desemba 28, mwaka jana, akiwa mmiliki wa nyumba aliruhusu mkutano kati yake na Ludovick kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya ugaidi,” alidai Rweyongeza.

Hakimu Katemana, alisema washtakiwa hawataruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba kuwasilisha hoja kwa ajili ya mteja wao lakini hakimu alikataa kufanya hivyo.

“Kaa chini, mwenye mamlaka ya mwisho hapa mahakamani ni mimi, kwa leo nina majukumu mengine sitaweza kusikiliza hoja zenu, nitawasikiliza Aprili 3 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa, washtakiwa mtaendelea kuwepo rumande,” alisema Katemana.

Mawakili wanaomtetea Lwakatare ni Tundu Lissu ambaye hakuwepo mahakamani, Kibatala, Profesa Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Mabare Marando wakati mshtakiwa Ludovick hana wakili wa kumtetea.

Akizungumza nje ya mahakama, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe huku mbwa wakiwa wamezingira eneo hilo, aliwaomba wanachama kuwa na utulivu, wakati masuala ya kisheria yakifuatiliwa.

“Makamanda mnatakiwa kujua uonevu huu anaofanyiwa Lwakatare, una mwisho na yeye si wa kwanza kufanyiwa haya hivyo si jambo la ajabu, mwisho wa mambo haya ni kufanya mabadiliko,” alisema Mbowe na kuwataka watawanyike katika eneo hilo.

Awali Machi 18, mwaka huu washitakiwa hao walipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mchauro na kusomewa mashtaka yanayofanana na hayo.

Hakimu Mchauro, aliwauliza washitakiwa kama wana kitu cha kusema dhidi ya mashtaka yanayowakabili, wote walikana mashtaka.

CREDIT: http://mtanzania.co.tz


Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top