BAADHI ya abiria na wamiliki
wamabasi katika halmashauri ya manispaa ya Songea wameulalamikia uongozi wa
manispaa hiyo kwa kushindwa kukifanyia matengenezo kituo kikuu cha mabasi cha
mjini Songea ambacho kimekithiri kwa kuwa na mashimo mengi na kusababisha
magari yanayoingia na kutoka kuharibika yakiwa kwenye kituo hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
baadhi ya abiria walisema kuwa hali ya kituo hicho cha mabasi ni
mbaya kwani katikati ya kituo kuna mifereji ambayo imekuwa ikipitisha maji wakati
mvua na maeneo mengine kuna madimbwi yaliyojaa maji ambapo magari yanapita kwa
taabu
Kuruthum Athuman mkazi wa kijiji
cha mtwara pachani wilayani namtumbo ameuomba uongozi wa halmashauri hiyo kuona
umuhimu wa kuchukua hatua za haraka za kukifanyia matengenezo kituo hicho
ambacho kwa muda mrefu ni kibovu na kusababisha wakati mwingine magari kukwama
katikati ya kituo hicho.
Adam Kumburu mkazi wa Ruhuwiko
wilayani Mbinga ameeleza kuwa kutokana na ubovu wa kituo cha mabasi hasa kwa
nyakati za masika abiria wamekuwa wakilazimishwa kupanda mabasi wakiwa nje ya
kituo hicho kwa sabababu mvua zinapokuwa zinanyesha kituo hicho kimekuwa
kikijaa tope jambo ambalo limekuwa likionekana kuwa ni kero kubwa kwa abiria.
Kwa upande wao baadhi ya wamiliki
wa mabasi yanayotoa huduma ya kusafirisha abiria kutoka Songea kwenda Mbinga na
kutoka Songea kwenda jijini Dar es Salaam wamesema kwa masharti ya
kutotajwa majina yao kwenye blog kuwa kituo cha mabasi cha mjini Songea ni kibovu
sana na kina mashimo mengi ambayo husababisha magari yanayoingia na kutoka
kwenye kituo hicho kutaka spiringi na kuwepo uharibifu wa mara kwa mara kwa
baadhi ya vipuri vya magari yao.
Walisema kuwa pamoja na kuwepo
uharibifu wa magari yao na kutoa malalamiko ya mara kwa mara bado halmashauri
inaendelea kukusanya ushuru wa kuegesha magari kwenye kituo hicho kila siku
mfano magari madogo (taksi) hutozwa shilingi 500/= kwa siku moja, magari
kuanzia tani tatu hadi tani kumi hutozwa kiasi cha shilingi 1000/= kwa siku kwa
kila gari linaloegeshwa kituoni hapo na magari makubwa kuanzia tani kumi hadi
tani kumi na tano linatozwa kiasi cha shilingi 2000/= kwa siku moja.
Walifafanua kuwa kwa wastani
halmashauri ya manispaa hiyo imekuwa ikipata mapato makubwa kutokana na
kuegesha magari kutoka katika kituo kikuu cha mabasi cha Songea kwani ni zaidi
ya magari kati ya hamsini na sabini kwa siku yanaingia kituoni hapo na kutozwa
ushuru wa maegesho. Hivyo wameumba uongozi wa halmashauri hiyo kuwa fedha zinazokusanywa
kutokana na maegesho ndiyo zitumike kufanyia ukarabati wa kituo hicho ambacho
ni kibovu kwa muda mrefu.
Walisema kuwa wameshangaa kuona
zimeletwa kokoto tangu miezi miwili iliyopita na kurundikwa katikati ya kituo
cha mabasi na mpaka sasa hakuna kinachoendelea na inaonekana kuwa kokoto hizo
zimeletwa kwa kuhifadhiwa kwa muda na sio kwa ajili ya matengenezo ya kituo
hicho kwani zingeletwa kwa matengenezo ya kituo hicho halmashauri ingekuwa
imeshaanza kufanya kazi hiyo lakini kokoto hizo zimekuwa zikisababisha mabasi
kuegeshwa kwa taabu.
Hata hivyo mkurugenzi wa
halmashauri ya manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alipohojiwa ofisini kwake kuhusiana na tatizo la ubovu wa kituo cha mabasi cha mjini Songea
alikiri kuwepo kwa tatizo hilo lakini aliwataka wakazi wa mjini songea pamoja
na wamiliki wa mabasi kuwa watambue kuwa mara zote ujenzi mchakato hivyo kwa
sasa wanatafuta vifaa mbalimbali na
wanaangalia uwezekano wa kupata lami kwani lengo kubwa la manispaa yake ni
kukifanyia matengenezo kituo hicho kwa kiwango cha lami.
Alisema kuwa kokoto zilizomwagwa
kwenye kituo hicho zimeletwa kwa msaada toka kampuni moja ya ujenzi wa barabara
mkoani Ruvuma hivyo kwa sasa hivi halmashauri yake bado inashughulikia zabuni
ya kumpata mtu wa kukijenga kituo hicho na amewataka kuwa wavumilivu na si
vinginevyo.
Post a Comment