Hili ni moja ya Ghuba lililopo pembezoni ya Mjia wa Songea
Pichani hapo juu ni ghuba lililopo Mtaa wa Sovi barabara iendayo kituo kikuu cha Polisi likiwa limejaa uchafu .
Wafanya biashara wa Mabucha ya Nyama na wauza Viungo wakiendelea na
biashara huku pembeni kukiwa na hali ya uchafu uliokithiri wasiwe na
wasiwasi.
.......................................................................
.......................................................................
Na Nathan Mtega,Songea
BAADHI ya wakazi wa
halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
wamelalamikia kukithiri kwa uchafu katika maeneo yote ya Manispaa hiyo na
kusababisha maghuba ya kuhifadhia taka kufurika kwa muda mrefu yakiwemo
yanayozunguka maeneo ya soko kuu,Majengo na kituo kikuu cha mabasi cha mjini
Songea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa mazingira ya usafi kwa ujumla katika
Manispaa ni mabaya na yanaweza yakaleta madhara makubwa ya kiafya ikiwa hali
hiyo haitachukuliwa hatua za haraka na maafisa afya wa Manispaa hiyo kwa sababu
baadhi ya maghuba yamefurika na kutoa harufu kali.
Walisema kuwa ni muda
mrefu hali hiyo ya uchafu imeendelea kuwepo na hakuna jitihada zinazofanyika kuiondoa
hali hiyo ambayo ni kero kubwa kwa wakazi walio wengi wa Manispaa hiyo licha ya
kuwa wamekuwa wakilipa ushuru wa usafi wa mazingira kila mwezi.
Wakizungumza Sebastiani
Komba na Elizabeth Luambano wakazi wa Bombambili walisema kuwa ni vyema
halmashauri ya Manispaa hiyo ikachukua hatua za haraka za kuiondoa adha hiyo
ambayo imekuwepo kwa muda mrefu huku Adam Haule na Edson Kumbuka wakazi wa
Majengo wakisema kuwa maghuba ya kuhifadhia taka yaliyopo yamefurika kupita
kiasi na watoto wakicheza kwenye maghuba hayo hali ambayo inaweza
ikawasababishia madhara.
Naye Seleman Said mfanyabiashara
wa soko kuu alielezea kusikitishwa kwake na hali ya kukithiri kwa uchafu ndani
ya eneo la soko kuu ambamo kuna ghuba la kuhifadhia taka ambalo ni muda mrefu
gali la kuzoa taka halijafika kuchukua taka taka zilizofurika kwenye ghuba hilo
na Rashid Husein wa kituo kikuu cha mabasi cha mjini Songea alisema kuwa taka
taka zilizopo kwenye ghuba ambalo lipo kando kando mwa kituo hicho zimekuwa
kero kwa wasafiri na wapiti njia.
Afisa afya wa
Manispaa ya Songea Maxmilian Mahundi alipojohojiwa na mwandishi wa habari kuhusiana na hali
hiyo alikataa kusema chochote kwa madai kuwa yeye siyo msemaji hata hivyo jitihada
za mwandishi wa habari zilimtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Nachowa Zacharia ambaye
alikiri kukithiri kwa uchafu katika halmashauri hiyo.
Alisema kuwa
halmashauri ya Manispaa ya Songea ina magari mawili tu ambayo ni chakavu na
yana zaidi ya miaka ishirini tangu yaliponunuliwa huku mahitaji ya magari mapya
kwa ajili ya kuzoa taka ni sita ambayo yana uwezo wa kubeba taka tani ishirini
kila moja na kijiko kimoja cha kuzolea taka badala ya kutumia vibarua ambao
wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kutumia vitendea kazi duni.
Aidha amewahimiza wakazi
wa Manispaa kuendelea kulipa ushuru wa usafi kwa kila kaya ambayo ni shilingi
150 kwa kila siku ili kupunguza adha iliyopo ya uchafu uliokithiri kwenye maeneo
mengi ya Manispaa hiyo
Post a Comment