Na Gideon Mwakanosya, Songea.
MWALIMU mmoja wa jinsia ya kike aliyefahamika kwa jina moja la Kahimba wa shule ya msingi ya Kambarage iliyopo Kata ya Msamala katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma amajeruhiwa vibaya kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili na kundi linalodaijwa kuwa ni la wanafunzi wa shule hiyo ambao wanadaiwa kuwa na hasira baada ya walimu wengi wa shule hiyo kutoonekana eneo la shule kufuatia mgomo wa chama cha Walimu (CWT).
Akizungumuza na waandishi wa habari hizi Mjini Songea mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kambarage Adolfina Ndunguru alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alidai kuwa ni udhalilishaji mkubwa kwa mwalimu kupigwa na wanafunzi.
Ndunguru alisema kuwa yeye pamoja na walimu wenzake hawakuweza kufika kwenye eneo la shule kwa kuwa wao ni walimu ambao wamekubaliana kugoma kutokana na Serikali kushindwa kutimiza ahadi yao wanayodai.
Alifafanunua kuwa inadaiwa kundi la wanafunzi lilipomuona mwalimu Kahimba kwenye eneo la shule hiyo lilimvamia na kuanza kumpiga mawe sehemu mbalimbali za mwili na baadaye alifanikiwa kukimbia.
Kwa upande wa baadhi ya walimu wa shule za msingi,Sekondari na Chuo cha Ualimu cha Songea kilichopo Manispaa ya Songea ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa mgomo utaendelea mpaka Serikali itakapo ridhia kuwalipa madai yao hasa ikizingatiwa kuwa wao wanafanyakazi katika mazingira magumu.
Waandishi wa habari walifanikiwa kutembelea baadhi ya shule za Msingi na sekondari ambazo zilikuwa hazina walimu kabisa na kwamba wanafunzi wa shule hizo wakiwa wamezagaa mitaani huku wakiinung`unikia Serikali kwa kuto watendea haki walimu wao ambao alikuwa wakiwaandaa wanafunzi katika Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi na sekondari.
Shule zilizotembelewa na waandishi wa habari ambazo hazikuwa na walimu kabisa ni Shule za Msingi za Matarawe, Mwembechai, Sabasaba, Mkombozi, Kawawa, Mfaranyaki, Majengo, Songea, Kambarage, Msamala na Majimaji na shule za sekondari za matarawe, Mfaranyaki, Shule ya wavulana Songea na Shule ya wasichana songea.
Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Majimaji Tamimu Ajali anayesoma darasa la tano ameiomba Serikali kuharakisha kutekeleza madai ya walimu wanayodai kwani bila kufanya hivyo kunauwezekano mkubwa wa kushuka kwa kiwango cha Elimu hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi wapo kwenye maandalizi ya kufanya mitihani.
Tamimu alisema kuwa ni vyema serikali ikatambua umuhimu wa mwalimu kwa kumuuongezea mshahara sawa na taaluma zingine muhimu kwa mfano. Wanajeshi, Madaktari,Wauguzi na wahudumu wa afya.
Afisa Elimu wa halmashauri ya Manispaa ya Songea Fulgensi Mponji amethibitisha kuwepo kwa mgomo huo wa walimu amabapo alisema Manispaa hiyo ina shule 72, Sekondari za Serikari 23, Shule za seskondari za binafsi 13 ambazo idadi kubwa ya walimu hawakuwepo kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema kuwa tayari ameshawaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na waratibu Elimu kata wote kukutananao katika shule ya msingi Mfaranyaki kwa lengo kuwakutanisha walimu ili kuzungumzia namna ya kutatua tatizo hilo.
Naye Katibu wa chama cha walimu mkoa wa Ruvuma Luya Ng`onyani alisema kuwa mgomo huo ni halali na umezingatia sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kifungu cha 80 (1) ambapo hatua ya kwanza CWT kwa niaba ya wanachama tayari imetekeleza kutangaza mgogoro wa siku 30 kwa kujaza fomu CMA No: 1.
Post a Comment