Loading...

MwanaHalisi kufungiwa: Ni jamii ya wa-Tanzania au ya Wagagagigikoko? - Prof. Mbele


Nimekuwa hapa Tanzania kwa wiki sita, na nimesoma nakala za MwanaHalisi zilizotajwa hapa. Nimejumuika na wananchi katika kujadili mambo mengi, likiwamo suala la ripoti na uchambuzi wa MwanaHalisi. 

Kila mahali nilipopita, kama vile Tanga, Arusha, Dar es Salaam, na Songea, wananchi wanalipenda na kuliheshimu gazeti la MwanaHalisi. Mhariri Saeed Kubenea anaheshimiwa na kushukuriwa na wananchi kwa kazi yake anayoifanya kwa umakini. Huo ndio mtazamo wa wananchi, nilivyoshuhudia. Sasa serikali inavyodai kuwa MwanaHalisi halina tija kwa jamii, lazima niulize ni jamii gani hiyo? Ni jamii ya wa-Tanzania au ya Wagagagigikoko?

Kitendo cha
serikali kulifungia gazeti hili ni kitendo cha uchochezi, kwa maana kwamba kitawaudhi au watu. Kama serikali inadhani kitendo hiki kitawaridhisha wananchi, itafakari upya.

Serikali haikatazwi kuandika makala ndefu kwenye magazeti yake, kukanusha taarifa zinazochapishwa na MwanaHalili. Ingekuwa na utaratibu wa kufanya hivyo, na kuzimisha hoja za MwanaHalisi kwa hoja, ningeiheshimu hii serikali. Lakini kwa vitendo hivi vya kutumia mabavu, serikali inajivunjia heshima mbele ya jamii.

Siku za karibuni, MwanaHalisi imekuwa ikiripoti habari za Dr. Ulimboka. Kitendo cha kulifungia gazeti hili kinatatanisha na kuzua masuali. Mungu amemnusuru Dr. Ulimboka. Wengi tunamwombea apone, atupe taarifa zaidi za yale yaliyompata. Tunahitaji kujua.

Sasa je, kama serikali inasema taarifa za MwanaHalisi ni uzushi, je serikali inapangia kumzuia Dr. Ulimboka asiwaeleze wananchi mambo hayo?

Serikali ingekuwa na busara, ingetafakari sana masuala haya ya Dr. Ulimboka kama yalivyoripotiwa na MwanaHalisi. Kulizuia gazeti hili, nahisi kutaimarisha dhana iliyozagaa katika jamii kwamba serikali inahusika katika shambulio dhidi ya Dr. Ulimboka. Inawezekana serikali haihusiki, lakini vitendo hivi vinaweza kuwa ni vya hasara kwa serikali yenyewe.

Nimalizie kwa kusema kwamba naudhika na vitendo vya kuhujumu haki yangu ya kusoma ninachotaka kusoma. Ni mtu mzima na nina akili zangu. Naweza kuchambua chochote ninachosoma. Serikali inapozuia gazeti au kupiga marufuku kitabu naona
inawatukana wananchi, kwamba hwawana akili ya kusoma na kuchambua mambo. 




Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright songeayetu.blogspot.com | Designed By JUNGUKUU.US
Back To Top